Wednesday, April 11, 2012

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA KANUMBA AFIKISHWA MAHAKAMANI

Msanii wa kike wa filamu Tanzania Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu,amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya msanii mwingine wa filamu Marehemu Steven Kanumba.

Amefikishwa mahakamani ikiwa ni siku nne, tangu alipokamatwa mara baada ya kifo cha msanii huyo ambaye inaaminika kuwa walikuwa na uhusiano wa Kimapenzi.

Mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam,Bi Augustina Mbando,Elizabeth Michael Kimemeta ajulikanaye kama Lulu kwa jina la Usanii,aliwasili mahakamani hapo akiwa chini ya Ulinzi mkali wa askari Polisi waliokuwa wamevaa kiraia na wengine wakiwa wamejihami kwa silaha.

Mara baada ya Kufikishwa mahakamani,upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa serikali Bi Elizabeth Kaganda ulimsomea shtaka moja ambalo ni la mauaji, kosa ambalo ni kinyume cha sheria ya kanuni ya adhabu kifungu cha 196.

Wakili huyo wa serikali Bi Elizabeth Kaganda,alidai mbele ya mahakama kuwa mnamo tarehe 07 mwezi April mwaka 2012,katika eneo la Sinza Vatican,msanii Elizabeth alimuua msanii Steven Kanumba.

Akiwa amevalia gauni kubwa lijulikanalo kama dera lenye rangi ya Njano mtandio wa rangi ya waridi na kandambili nyekundu mshtakiwa alionekana kutokuwa na wasi wasi pamoja uzito wa tuhuma za mauaji anayokabiliwa nayo huku akijibu maswali kadhaa kuhusu wasifu wake.

Msanii huyo alikanusha kuwa na umri wa miaka 18 baada ya kuulizwa ,ambapo yeye amesisitiza kuwa ana umri wa miaka 17, hii ikiwa ni tofauti na habari ambazo zimekuwa zikiripotiwa kuhusu umri wa msanii huyo ambaye sasa anatambulika kama mshtakiwa.

Kesi hii ya mauaji inatajwa kwa mara ya kwanza na mshtakiwa hakutakiwa kukiri wala kukana mashtaka.

Upande wa mashtaka umeieleza mahakama kuwa kesi bado iko kwenye upelelezi ambapo inatarajiwa kutajwa tena April 23 mwaka huu.

Mshtakiwa amepelekwa rumande hadi siku hiyo wakati kesi hii itakapotajwa tena.

Kwa upande mwingine tukio la kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo kumefanywa kwa usiri mkubwa na kufanya waandishi wa habari wengi wameshindwa kufuatilia kwa karibu tukio lenyewe.

Kufikishwa mahakamani kwa msanii huyo na kusomewa shtaka la mauaji ya Kanumba kumetokea siku moja baada na Marehemu Steven Kanumba kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni.

Mazishi yake yalichukua sura ya kitaifa kutokana na umaarufu aliojijengea msani huyo katika jamii ya watanzania na hata nchi za nje.

No comments:

Post a Comment