Saturday, October 31, 2015

LINI MAGUFULI ATATEUA MAWAZIRI? MAGUFULI AWAPASHA WANAFIKI, HALI TETE ZANZIBAR MAGAZETI YA LEO.

Magufuli awapasha wanafiki, Vijana wa UKAWA waachiwa kwa dhamana, Tume ya uchaguzi yamaliza kazi rasmi. Pitia dondoo za magazeti;

GAZETI LA MWANANCHI
SATURDAY, OCTOBER 31, 2015

Kaa chonjo, saa mbaya




Rais Mteule Dk John Magufuli
Rais Mteule Dk John Magufuli 
By Julius Mathias na Beatrice Moses, MWANANCHI
Dar es Salaam. Ni kama alikuwa akisema “kaa chonjo, saa mbaya” wakati Rais Mteule Dk John Magufuli alipohutubia kwa mara ya kwanza tangu atangazwe kuwa mshindi wa mbio za urais.
Dk Magufuli, ambaye alikuwa akihutubia wafuasi wa CCM nje ya ofisi ndogo za chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi wa urais, alituma salamu hizo kwa watendaji serikalini na hata kwa wanachama wa CCM aliowaita wanafiki.
Waziri huyo wa zamani wa Ujenzi aliwataka watendaji wa Serikali wanaotumia ofisi za umma kama vijiwe; kwa manufaa yao binafsi; wasiojali wananchi; na wanaofanya kazi kwa mazoea, kujiandaa kuondoka.
“Rais wangu, mwenyekiti wangu Jakaya Kikwete utanisamehe kwa hatua nitakazozichukua kwa watu uliowalea wakati wa utumishi wako, na hawa ndiyo waliokukwamisha,” alisema Dk Magufuli ambaye alikuwa akijinasibu kwa uchapakazi wakati wa kampeni zake.
“Watu wanafanya kazi kwa mazoea. Wengine hawajali kabisa mahitaji ya wananchi wanaofika kwenye ofisi wanavyotaka. Utanisamehe Rais wangu, hawa ndiyo waliochangia kukukwamisha. Kwenye Serikali yangu wajiandae kuondoka.”
Dk Magufuli alikuwa akiwashukuru wanachama na wafuasi wa CCM muda mfupi baada ya kukabidhiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) cheti cha ushindi katika uchaguzi wa Rais kwenye hafla iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee. Wakati hali ya kisiasa Zanzibar ikiwa tete, hakukuwapo na viongozi wengi kutoka visiwa hivyo, zaidi ya Samia Suluhu Hassa, ambaye ni Makamu Mteule wa Rais.
Dk Magufuli alisema amezunguka nchi yote na kukutana na wananchi ambao wamemueleza kero mbalimbali.
“Nimegundua wengi wana matumaini makubwa sana na mimi. Binafsi, ninauona ugumu wa kazi iliyo mbele yangu, lakini nitaifanya na nafahamu kuwa nitagusa maslahi ya wengi, hivyo wajiandae,” alisema Dk Magufuli, ambaye ameibuka na ushindi wa kura 8,882,935, ikiwa ni tofauti ya zaidi ya kura milioni 2.8.
Akiwa jukwaani alimueleza Rais Kikwete kwamba moja ya vitu vilivyomkwamisha kuwaletea maendeleo makubwa wananchi ni watendaji wabababishaji waliokuwemo kwenye ofisi nyingi wakati wa utawala wake na akaahidi kukabiliana vilivyo na changamoto hiyo.
Katika kufikia lengo hilo, alisema ingawa kwa wakati wote yeye na mgombea mwenza walikuwa wakiinadi ilani ya CCM, katika kuliletea Taifa maendeleo kila mtu anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa uaminifu.
Ili kusisitiza juu ya azma yake ya kusimamia utendaji serikalini, Dk Magufuli alisema siku atakapoapishwa, ataanza kazi mara moja kwani tayari ameshatembezwa sehemu zote za Ikulu na Rais anayemkabidhi kijiti cha uongozi, na hivyo kilichobaki ni utekelezaji wa mipango yake kwa vitendo.
“Nimeona nilisema hili mapema ili lisiniletee kiungulia.”
Dk Magufuli, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Kilimo, Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo pamoja na Wizara ya Ujenzi, alikumbusha changamoto nyingi alizokutana nazo sehemu alizopita na kubainisha kuwa jukumu zito alilokutana nalo ni kuwasafisha watendaji ambao hawawajibika ipasavyo.
Alisema kazi hiyo ilimuweka kwenye wakati mgumu na kuahidi halitajirudia akiwa madarakani.
Aliwashukuru Watanzania kwa uaminifu waliouonyesha kwake na mgombea mwenza, Samia Hassan Suluhu kwa kuwapa ridhaa ya uongozi kwa miaka mitano ijayo na kueleza kwamba ushindi huo si wa CCM pekee bali wananchi wote kwa jumla.
Alisema hiyo inatokana na ukweli kwamba licha ya kwamba kwenye baadhi ya maeneo wapinzani walishinda nafasi za udiwani na ubunge, kwenye urais walimpa yeye ili awe na wajibu wa kuwatumikia kwenye nafasi hiyo ya juu zaidi katika uongozi wa nchi.
Pamoja na changamoto zote zilizojitokeza wakati wa mchakato wa uteuzi mpaka kampeni, Dk Magufuli alisema kuna wajibu wa kuijenga upya CCM kwani kuna mambo yanakwenda ndivyo sivyo na yasipofanyiwa kazi mapema yatakiangusha chama hicho.
“Kwenye kampeni za mwaka huu tumepata changamoto nyingi sana na baadhi zilitoka ndani ya wana-CCM. Hakuna haja ya kuwa na idadi kubwa ya wanachama wakati kuna wanafiki,” alisema Dk Magufuli, ambaye kwa mujibu wa utaratibu wa chama hicho, Rais hutakiwa kuwa mwenyekiti.
“Samahani Rais wangu. Ukiona mnafiki, mfukuze mara moja. Ni rahisi kupambana na adui aliye nje kuliko wa ndani. Hakuna haja ya kuwa na wanachama wengi wanafiki, ni bora wabaki wachache lakini waaminifu.
“Nisiposema nitakuwa mnafiki, msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Watubu wajirekebishe. Ni heri mara kumi kuwa na mpinzani kutoka nje kuliko ndani ya chama. Mipango yenu mtaipanga mchana usiku wataitoa nje, ni afadhali uwe na mchawi atakuroga ufe kuliko mnafiki ndani.”
Dk Magufuli aliwahi kutoa kauli kama hiyo wakati wa kampeni zake aliposema kuwa baadhi ya wanachama walikuwa naye mchana, lakini usiku walikuwa Ukawa.
Huku akishangiliwa, Dk Magufuli alimgeukia Kikwete na kusema: “Wewe ni mwenyekiti, lakini ulikaa na wanafiki ndani ya CCM. Hao ndiyo wametufanya wakati mwingine tufike hapa tulipofika.”
Hata hivyo, Dk Magufuli aliwataka wale wote walioasi warejee kwenye chama ili kwa pamoja, waweke mikakati itakayokiimarisha chama kinachoongoza dola wakati kikiwatumikia wananchi waliokiamini kwa moyo mkunjufu.
Pamoja na watu wengine, aliwashukuru wasanii waliozunguka naye mikoani wakati wa kampeni za kujinadi kwa mchango wao mkubwa ambao alisema ulifanikisha ushindi unaompeleka Ikulu.
Kuanza kazi haraka
Dk Magufuli aliwahakikishia wananchi kuwa mara baada ya kuapishwa, ataanza kazi kwa kuwa hakuomba nafasi hiyo kwa majaribio bali kuwatumikia wananchi kwa dhati.
Pia ameomba ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi ili waweze kufanikisha utekelezaji wa ilani kwa yale ambayo ameahidi wakati wa kampeni yeye na Makamu Rais Samia Suluhu Hassan, ili waweze kutimiza wajibu wa kuwatumikia bila kinyongo na kuyatimiza yake waliyoahidi wakati wa kampeni.
“Kwa hiyo niwaombe ndugu zangu Watanzania wote bila kujali vyama vyetu, tunaomba sana ushirikiano wenu , tusipopata ushirikiano wetu hatuwezi kuyatimiza kwa wakati. Tusipopata ushirikiano mzuri kutoka kwenu, mtatuchelewesha,” alisema.
Alisema kero walizoziona kwa wananchi ni maji, umeme, miundombinu, ambazo alisema wananchi wanataka zitatuliwe haraka.
Amsifu JK
Dk Magufuli alimsifu Rais Jakaya Kikwete akisema: “Nataka niseme mheshimiwa Rais una moyo wa pekee, Mungu akujalie sana. Viongozi wengi Afrika wanapokaribia kuondoka madarakani wengine huwa wanatengeneza hata katiba tofauti ili waendelee kubaki madarakani, lakini wewe upo tayari kuondoka hata leo.”
Dk Magufuli alisema anaamini kwamba wananchi wataendelea kumuombea kwa kuwa amethamini Tanzania kwanza, hivyo ataendelea kuhitaji busara zake pale itakapobidi.
Rais Kikwete
Awali, Rais Kikwete alitupa kijembe kwa baadhi ya makada wa CCM waliokihama chama hicho baada ya kutemwa kwenye kura za maoni, akisema hawakuweza kutimiza ndoto zao.
Kikwete alisema nafasi hiyo haipatikani kimasihara na kwamba juhudi kubwa hufanywa kabla ya kupatikana kwa mteule ambaye atatumikia wananchi bila kujali itikadi zao, dini wala kabila.
“Tumempata Rais mteule. Sasa tushirikiane kuijenga nchi yetu. Kulikuwa na wengi waliojitokeza hata wengine wakathubutu kuhama chama wakiamini wameonewa, lakini hata walikokwenda wameukosa urais,” alisema Kikwete.
“Tumempata mbadala wangu, mlisema mimi mpole sasa huyu ni tingatinga.”
UN yampongeza
Katika hatua nyingine, salamu za pongezi zimeanza kumiminika baada ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon kuipongeza Tanzania kwa kufanya uchaguzi wake kwa amani na kusema huo ni mfano kwa nchi zinzotekeleza demokrasia ya kweli.
Katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Ki-moon ameeleza kufurahishwa kwake na utulivu ulioonyeshwa na Watanzania wakati wote, kuanzia upigaji kura, kuzihesabu mpaka utangazaji wa matokeo.
“Uvumilivu mliouonyesha umethibitisha uzingatiaji wenu wa demokrasia, amani na utulivu. Kilichotokea Zanzibar kinavuta macho yangu pia, napenda kushauri njia za maridhiano ya kupata muafaka kwa changamoto yoyote inayojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu,” inasema taarifa hiyo. SOMA ZAIDI KUPITIA Gazeti la  MWANANCHI

No comments:

Post a Comment