Monday, September 27, 2010

Papa wa Misri awaomba radhi Waislamu

Kiongozi wa kikiristo wa madhehebu ya Copti nchini Misri ameomba radhi kwa matamshi "yasiofaa" yaliyotolewa na askofu aliyoonesha kuwa na wasiwasi na baadhi ya aya za Quran.

Papa Shenouda III alisema kupitia televisheni ya taifa, " Ninaomba samahani sana kuwa hisia za ndugu zangu wa kiislamu zimeumizwa."

Awali, askofu Bishoy alisema- tofauti na imani za Muislamu- baadhi ya aya za Quran huenda ziliongezwa baada ya kifo cha Mtume Muhammed.

Mamlaka ya kiislamu ya al-Azhar nchini humo yamesema matamshi hayo yanatishia usalama wa kitaifa.

Imam Ahmed al-Tayyeb katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumamosi na al-Azhar, moja ya kituo muhimu ya mafunzo ya kidini ya madhehebu ya Sunni, " Tabia ya namna hii haifai na inatishia usalama wa taifa katika wakati ambao ni muhimu kuulinda."

Alikuwa akijibu baada ya taarifa kutolewa na vyombo vya habari vya Misri ambapo askofu Bishoy, ambaye ni wa pili kwa nafasi za upadri katika kanisa hilo la Copti, alipohoji aya za Quran kupinga Umungu wa Yesu Kristo.

Askofu huyo aliripotiwa akisema aya hizo ziliwekwa na mmoja wa maswahaba zake Mtume Muhammed baada ya kifo chake.

Waislamu wanaamini kuwa aya zote za Quran zilidhihirishwa kwa mtume kupitia malaika Jibril na ni neno la Mungu lisiobadilika.

Papa Shenouda alisema katika mahojiano ya televisheni siku ya Jumapili, " Midahalo ya imani za kidini ni mwiko, mwiko kabisa."

Aliongeza, "Suala la kuibua mijadala hiyo si sawa, na kulizungumzia zaidi haifai."

Ijapokuwa Waislamu na Wacopt wa Misri aghlabu huishi kwa amani, wasiwasi unazuka juu ya kujengwa makanisa mapya na matukio ya kubadili dini.

Idadi ya wafuasi wa madhehebu ya Copt ni kuanzia asilimia sita hadi 10 ya raia milioni 80 nchini humo na hulalamika juu ya ubaguzi unaofanywa na taifa hilo.

No comments:

Post a Comment