Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Sepp Blatter amesema kuwa amesikitishwa na yale yaliyofanyika siku ya Jumamosi usiku katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo mjini Nairobi,tukio lililosababisha vifo vya watu saba na wengine wengi kujeruhiwa.
"Napenda nieleze kusikitishwa kwangu na napenda nitangulize rambi rambi zangu kwa mashabiki wa soka nchini Kenya,na zaidi kwa jamii na marafiki kufwatia vifo hivi," alisema Rais wa FIFA.
"Nafahamu kwamba uchunguzi umeanzishwa. Lazima juhudi zifanywe ili chanzo cha tukio hili baya kijulikane kwa nia ya kuzuia hali hii kutokea kwenye uwanja wa Nyayo tena."
Ni hapo Jumatatu tu, ambapo FIFA ililitaka shirikisho la soka nchini Kenya FKL kuelezea mazingira, yaliyosababisha mkasa huo kutokea.
Shirikisho la FKL, limepiga marufuku mechi zozote kufanyika katika Uwanja wa Nyayo na ule wa City, hadi watimize masharti ya usalama kuambatana na kanuni za FIFA.
Mkasa huo wa Jumamosi ulitokea wakati mashabiki wa mahasimu wa jadi AFC Leopards na Gormahia waking'ang'ana kuingia uwanjani.
Ilikuwa ni katika pambano la ligi ya kitaifa.
No comments:
Post a Comment