Thursday, November 11, 2010

FIFA YAMUONGEZEA PESA OBILALE WA TOGO.

Mlinda mlango wa timu ya taifa ya Togo Kodjovi Obilale atapatiwa dola100,000 kutoka Shirikisho la Soka Duniani- Fifa baada ya kujeruhiwa vibaya kwa risasi kabla ya kuanza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola mwezi wa Januari.
KODJOVI OBILALE.
Rais wa Fifa Sepp Blatter, alimwambia Obilale mwezi wa Septemba kwamba malipo ya dola 25,000 zitatolewa kutoka mfuko wa Fifa wa misaada ya kibinadamu.

Hata hivyo Shirikisho hilo la soka Duniani kwa sasa limeamua kuongeza kiwango hicho cha pesa.

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 25 alifanyiwa upasuaji kutokana na majeraha ya risasi alizopigwa mgongoni na tumboni kufuatia shambulio hilo.

Shambulio hilo lililotokea katika jimbo la Cabinda nchini Angola, lilisababisha watu wawili waliokuwemo katika kikosi cha Togo kupoteza maisha pamoja na dereva wa basi lililokuwa limewachukua.

Obilale bado hawezi kutembea ikiwa ni miezi minane tangu lilipotokea shambulio la risasi lililofanywa na waasi wanaotaka kujitenga kwa jimbo la Cabinda na bado anaendelea kutibiwa nchini Ufaransa.

Togo ilijitoa katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola baada ya shambulio hilo na ilifungiwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) kwa miaka minne kushiriki mashindano hayo.

Hata hivyo Fifa ilitengua adhabu hiyo.

Akiwa amekatishwa tamaa kwa kukosa msaada kutoka Caf na Angola ambao waliandaa mashindano hayo, Obilale alimwandikia barua Rais wa Fifa Blatter mwezi wa Agosti akimuomba msaada.

Blatter akamuahidi msaada kutoka mfuko huo wa Fifa wa misaada ya kijamii, pamoja na kumueleza Fifa haina dhamana na mashambulio ya Cabinda.

Obilale alieleza hadhari kukatishwa tamaa kwa kukosa msaada wa Caf na maafisa wa Angola baada ya shambulio hilo ambalo limekatisha matumaini yake ya kucheza soka.

Mlinda mlango huyo aliyekuwa akichezea klabu moja ya daraja la chini huko Ufaransa, hawezi kusogeza mguu wake wa kuume chini ya goti, pia mguu wake umekufa ganzi, lakini ana matumaini ataweza kutembea siku za baadae.

Kwa sasa anatumia kiti maalum cha kutembelea kuzunguka hapa na pale na amesema angekuwa na jina kubwa katika soka, basi matibabu yake yangekuwa tofauti na anayopatiwa sasa..

No comments:

Post a Comment