Thursday, September 23, 2010

JE ARSENAL WANAONEA WANYONGE?

Katika mechi tatu Arsenal wamefikisha jumla ya magoli 16. Walipocheza dhidi ya Braga ya Ureno walitikisa magoli mara sita, kabla ya hapo waliichapa Bolton Wonderers goli 4-1, awali Blackpool walipigwa 6-0.

Arsene Wenger anaamini timu yake imejengeka zaidi na itapata mafanikio, lakini amesikika akisema hivyo miaka kadhaa bila kuambulia kitu.

Maswali ambayo yanaibuka ni je Arsenal inaonea wanyonge? Wakipambana na timu kali kama Chelsea, Man U au Real Madrid na Barcelona watafurukuta kwa kasi hiyo waliyo nayo sasa?

Ni wazi kuwa safu ya ulinzi msimu huu imeimarika zaidi kuliko wakati Mikael Sylvestre na Sol Campbell na William Gallas walipokuwa wakicheza katikati. Lakini kama ni Arsenal kuonea wanyonge, iweje pasipo Robin van Parsie, Theo Walcott, Thomas Vermaelen, Abu Diaby na wengineo, bado wanaweza kufunga magoli sita katika mechi moja?

Huenda ni mapema sana kuhoji uimara wa Arsenal. Lakini meneja Arsene Wenger anasema ana imani kikosi chake kimejengeka na kipo tayari kukwaruzana na timu yoyote kubwa au ndogo.

Kwa jinsi walivyocheza mechi ya ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya dhidi ya Braga, Arsenal wanacheza soka ya kuvutia, lakini mara nyingi soka hiyo imegeuka kuwa maumivu wanapocheza na timu zisizokuwa na masihara mbele ya goli.

Na je Arsene Wenger amesikika mara ngapi akisema "chipukizi wake" watabeba kikombe au vikombe? Tunachoweza kufanya kwa sasa, ni kusubiri mwisho wa msimu.

No comments:

Post a Comment